Mapya haya; Sumu ya nyuki inavyoangamiza VVU
Wengi tunafuga nyuki, tunakula asali lakini hatujui kama nyuki wana faida zaidi ya hizi hapa.
Wanasayansi kutoka chuo kikuu cha tiba Washington, Marekani wamegundua
katika utafiti wao kuwa sumu iliyopo katika mwili wa nyuki iitwayo toxin
melittin inaweza kuvivunjavunja na kuviharibu virusi vya Ukimwi pasipo
kuacha madhara katika chembehai za mwili.
Habari hii imeelezwa katika taarifa ya tiba za dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi iliyotolewa mapema mwaka huu.
Watafiti hawa wanaeleza kuwa matokeo ya utafiti huu kufika katika hatua
kubwa inayoleta matumaini ya kupamba na VVU kwa kuweza kupata dawa ya
kupaka ya majimaji ndani ya uke itakayotumika kupambana na maambukizi ya
VVU.
Dk Joshua Hood anasema: “Matumaini yetu ni kwa maeneo ambayo hali ya
maambukizi yapo juu na vigumu kuzuilika, dawa ya majimaji mazito inaweza
kutumika kupaka ndani ya uke katika kuzuia maambukizi ya mwanzoni
kabisa.”
Sumu ya nyuki, melittin, imeonyesha uwezo wa kupambana na VVU kwa
kuvunja ganda linalomzunguka kirusi na virusi wengine kwa kulitoboa na
kuacha matundu.
Mwandishi mwandamizi wa makala za biokemia, Dk Samuel Wicline, Profesa
wa Biochemia wa Taasisi ya Russel Hornsby anafafanua kuwa kuwa vijipande
vidogo vilivyoshindiliwa vya sumu ya nyuki vimeonyesha kuwa na tabia ya
kuweza kuua chembe hai zenye saratani.
Anaeleza mtaalamu huyo kuwa hii si mara ya kwanza katika ugunduzi wa
tiba ya namna hii, kwani mwaka 2004 wanasayansi wa Croatia walitoa
taarifa yao katika jarida la sayansi ya chakula na kilimo kuwa mazao ya
nyuki, ikiwamo asali na sumu ya nyuki vina uwezo wa kutumika kutibu na
kuzuia saratani.
Chembehai za mwilini zenye afya huendelea kubaki salama pasipo kupata
madhara wakati wa tiba kwani sumu hiyo ya nyuki imetengenezewa na kitu
kama ngao ambayo ikikutana na seli za mwili hudunda na kwenda mbali bila
kujishikiza.
Hii ni kwa sababu ya seli za mwili ni kubwa kimaumbille kuliko sumu ya
melittin, wakati kwa virusi vya Ukimwi ni vidogo kuliko melittin, hivyo
ikikutana navyo ngao hiyo haiwezi kuzuia kirusi kidunde kwani ni
kidogo, hivyo kirusi hudakwa na melittin na kushikamana, hivyo kirusi
huweza kuharibiwa.
Dk Hood anaeleza kuwa vijipande vilivyoshibishwa na sumu ya melittin
huweza kushikamana na kirusi na kutoboa tundu katika ganda la kirusi na
kuchana ganda lote, hivyo kirusi huweza kuvunjwa.
Wakati tiba kwa kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU, yaani ARVs
zinafanya kazi kwa kuzuia uwezo wa virusi kujidurufisha, kwa tiba ya
melittin hushambulia sehemu muhimu ya kimaumbile ya virusi ambayo ndiyo
nguzo imara kwa virusi.
Tatizo katika tiba ya kuzuia uwezo wa kirusi kujidurufisha ni kuwa
maambukizi yanakuwapo na hayakomi mwilini, hivyo hayazuii maambukizi
kuwepo mwilini.
Baadhi ya vipande vya virusi vya Ukimwi vimepata uwezo wa kujibadili
hivyo kuzuia ufanyaji kazi wa ARVs na hivyo kuendelea kuzaliana na
kuvamia seli za mwili.
Mtaalamu huyo anaeleza: “Tunashambulia sehemu ya kimaumbile ya kiurithi
ya VVU, kinadharia, tunasema hakuna namna yoyote ya kirusi kuweza
kujibadili ili kukabiliana na mazingira mapya ya kujihami na
mashambulizi ya tiba hii ukilinganisha na mashambulizi ya ARVs’ kirusi
kitahitaji kuwa na ganda la kujikinga lenye ngozi ya tando mbili ili
kuweza kujibadilisha.
Dk Hood anaamini kuwa sumu ya nyuki iliyoshibishwa vijipande vya
melittin ina uwezo wa kitiba wa aina mbili katika kutibu na kuzuia, moja
ikiwa kutumika kama maji mazito ya kuweka ukeni (vaginal jelly) ili
kuzuia maambukizi ya VVU kuenea .
Tiba ya pili ni kutumika kwa maambukizi ambayo tayari yapo mwilini hasa
kwa maambukizi yaliyoleta usugu wa dawa, kinadharia ni kuwa kama sumu ya
melittin itadungwa mwilini na kuingia katika mzunguko wa damu inaweza
kuviangamiza virusi vya Ukimwi.
Anaeleza Dk Hood kuwa, “Kimsingi, vijipande hivi vya tiba vilivyotumika
vilianza kufanyiwa majaribio ya kimaabara miaka mingi iiliyopita ikiwa
kama zao la damu bandia ya kutengenezwa maabara.
Hata hivyo, haikufanya vyema katika kubeba na kusambaza hewa ya
oksijeni, lakini ikawa ikizunguka katika mzunguko wa damu ikiwa salama
mwilini na hivyo ilitupa mwanga wa kuweza kupata mbinu mpya ya kupambana
na maambukizi ya aina tofauti.”
Melittin inashambulia tando mbili za ngozi laini pasipo kutofautiana,
hii inaifanya melittin iwe dawa yenye uwezo wa juu kitiba katika
mapambano dhidi ya maambukizi VVU.
Virusi kama Hepatitis B (homa ya ini) na C ambavyo navyo vina ganda la
kuwakinga la namna hii navyo vinakuwa miongoni mwa virusi vinavyoweza
kuangamizwa na tiba ya melittin.
Pia, majimaji mazito (jelly) ya melittin pia huenda yakalenga mbegu za
kiume. Mtafiti Hood anaeleza kuwa inaweza kutumika kama dawa za kuzuia
mimba, hivyo kuwa kama njia ya uzazi wa mpango. Hata hivyo, bado
hawajalifanyia kazi.
Pia, wanaangalia uwezekano wa wenza wawili ambao mmoja wao
aliyeambukizwa VVU pale watakapohitaji kupata mtoto aliye salama, kwani
vijipande hivyo vya melittin ni salama kwa mbegu za kiume kwa sababu
hiyohiyo ni salama pia kwa seli za ukeni.
Dk Hood anasema bado ni mapema mno kwani mpaka sasa majaribio yote ni ya kimazingira ya kimaabara.
Mwananchi
Post a Comment