Lissu aigomea CCM:CHADEMA WAHAMIA DODOMA KUMUUNGA MKONO
WAKATI
viongozi mbalimbali wa CHADEMA wakiwasili mjini Dodoma kuungana na
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, katika rufaa ya kupinga ubunge
wake inayoanza kusikilizwa leo, mbunge huyo amekataa uamuzi CCM kutaka
kuifuta kesi hiyo.
Juzi CCM
kupitia kwa wakili wake, Godfrey Wasonga, iliwasilisha barua katika
Mahakama ya Rufaa Dodoma na nakala kwa Lissu ikiomba mahakama hiyo
kuifuta kesi hiyo.
Kwa mujibu
wa wakili huyo, sababu ya kuomba kufutwa kwa kesi hiyo ni walalamikaji
wote kujitoa na kuapa mahakamani kuwa hawakuwa tayari kuendelea na kesi
hiyo.
Taarifa
zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema kuwa viongozi kadhaa wa CHADEMA
wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod
Slaa, wajumbe wa Kamati Kuu na wabunge kadhaa wa chama hicho tayari
walikuwa wamewasili mjini Dodoma.
Hata hivyo, akizungumzia kesi hiyo, Lissu alisema kuwa hatakubali ‘withdrawal’ isipokuwa anataka ‘dismiss with cost’.
Lissu
alisema kuwa Wasonga atalazimishwa kulipa gharama kwa kuwa hati ya kiapo
cha Selema ni ya mwezi Juni 25, mwaka huu, na kwamba kutaka kuiondoa
siku mbili kabla ni uhuni.
Shabani
Selema na Paskali Hallu ni wanachama wa CCM wakazi wa kijiji cha
Makiungu, mkoani Singida, ambao walifungua kesi ya msingi ya kupinga
ubunge wa Lissu.
Lakini baada
ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kumtangaza Lissu kama mbunge
halali, walikubaliana na hukumu hiyo ya Aprili 27, mwaka huu.
Mara kadhaa
wananchi hao wamenukuriwa wakimlalamikia Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana, kuwa anawashinikiza kuendelea na rufaa hiyo licha ya kwamba
walishajitoa.
Akizungumza
na gazeti hili juzi, Wasonga, ambaye alikuwa akiwatetea wanachama hao
katika kesi hiyo, alisema kuwa baada ya kuwasiliana na wateja wake
walimwambia hawakuwa tayari kuendelea na kesi hivyo.
“Ni kweli walalamikaji wote wamejitoa na mimi kama wakili sioni haja ya kuendelea; nitakuwa namwakilisha nani?
“Niliongea nao jana hakuna; mwenye nia ya kuendelea na kesi,” alisema.
Rufaa hiyo
imepangiwa kusikilizwa katika Mahakama ya Rufani na Jopo la Majaji
watatu, Salumu Massati, Engela Kileo na Natalia Kimaro.
Kabla ya
kuanza kusikilizwa kwa rufaa hiyo, mahakama ilitarajiwa kusikiliza
pingamizi zilizotolewa na upande wa walamikiwa ambao ni Lissu na
jamuhuri za kupinga rufaa hiyo na jopo hilo la majaji litatoa maamuzi.
Tayari Lissu
alitoa hoja saba za kupinga rufaa hiyo, ambazo ni mkata rufaa Seleman
ambaye ndiye mlalamikaji namba moja kupinga kwamba hajakata rufaa kwa
hati ya kiapo ya Mei 24 mwaka huu.
Alisema hoja
nyingine ni notisi ya kiapo kutopelekwa kwa mjibu rufaa ambaye ni yeye
kinyume na masharti ya kanuni ya 84 (1) ya Kanuni za Adhabu za Mahakama
ya Rufaa Tanzania za mwaka 2009.
“Vile vile
nakala zote rekodi za rufaa hazijathibitishwa usahihi wake na wakata au
wakili kinyume na masharti ya Kanuni ya 96 (5) ya Kanuni za Mahakama ya
Rufaa Tanzania za mwaka 2009.
“Rufaa hii
pia imepitwa na muda wake kwa sababu hati ya ucheleweshaji iliyotolewa
na Msajili wa Mahakama Kuu haijasainiwa, haina tarehe wala muhuri
kinyume na Kanuni ya 90 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
za mwaka 2009,” alisema.
Lissu
aliongeza kuwa walalamikaji walitakiwa kukata rufaa siku sitini baada ya
notisi ya rufaa kutolewa na kwamba tarehe ya mwisho ya kukata rufaa
ilikuwa Julai 3 mwaka jana lakini rufaa hiyo ilikatwa Mei 7 mwaka huu.
“Hoja
nyingine ni kwamba rufaa hiyo si halali kwa kuwa imeacha nyaraka muhimu
ikiwemo maombi ya mwenendo wa shauri wa kusamehewa gharama za dhamana,”
alisema.
Lissu
alisema pia katika rufaa hiyo, amri iliyomshindisha kesi si halali kwa
kuwa haionyeshi tarehe ambayo amri hiyo ilitolewa kinyume na kanuni ya 9
ya Kanuni za Masijala za Mahakama Kuu za mwaka 2005.
Alisema pia
wakata rufaa wamesindwa kuwasilisha mahakamani hoja za maandishi za
kuunga mkono hoja za rufaa yao ndani ya siku 60 au kuomba muda wa
kuziwasilisha.
Pia hoja
nyingine ni kushindwa kuwasilisha hoja hizo za maandishi kinyume cha
Kanuni ya 106 (1), (2) na (9) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
za mwaka 2009.
Kesi ya
kupinga ubunge wa Lissu ilianza kusikilizwa Machi 12, 2012 na Jaji wa
Mahakama Kuu, Moses Mzuna, aliyetoa hukumu April 27, mwaka huu, na
kumtangaza Lissu kuwa mbunge halali wa Singida Mashariki kwa kigezo kuwa
hoja zote zilizotolewa na wanachama hao wa CCM hazitoshi kutengua au
kubatilisha ubunge wake.

Post a Comment