Header Ads

Sakata la Walimu wa Kike Kufanyishwa Mapenzi Usiku KICHAWI Lachukua sura mpya



SAKATA la walimu wa Shule ya Msingi
Nambaza, katika Wilaya ya Bunda, mkoani Mara,
kufanyiwa vitendo vya kishirikina na kutishiwa
maisha, limeendelea kuumiza vichwa vya
viongozi wilayani humo.
Viongozi hao, leo wanatarajia kukutana katika
kikao ambacho kitamshirikisha Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya, Ofisa Utumishi na Ofisa
Elimu wa Wilaya hiyo ili kujadili hatima ya
walimu wa shule hiyo ambao wote
wamefungasha mizigo yao na kutoweka kijijini
hapo wakihofia kuuawa na baadhi ya ndugu wa
watuhumiwa.
Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo, Bw. Ruben
Kaswamila, amesema kuwa kikao hicho pamoja
na mambo mengine, pia kitajadili tukio zima la
Nambaza ambalo ni la aibu na kushangaza ili
kuangalia uwezekano wa kuwahamisha walimu
wote wageni na kuwapangia vituo vingine.
"Kesho (leo) tutakuwa na kikao ambacho
kitamhusisha Mkurugenzi, Ofisa Utumishi na
mimi Kaimu Ofisa Elimu ili kujadili suala zima la
Nambaza na hatima ya walimu wa shule hiyo
waliodhalilishwa.
"Mwelekeo wa kikao ni kuwahamisha walimu
wote wageni na kuwapangia vituo vingine vipya
vya kazi kwani kuendelea kuwaacha hapo ni
kuwahatarishia maisha maana hata kisaikolojia
hawawezi kufundisha shuleni hapo kwa ufanisi,"
alisema.
Alisema uhamisho huo hautawahusu walimu
watatu wa shule hiyo, Bw. Sospeter Mafuru
ambaye ni Mwalimu Mkuu, Bw. Medard Munaku
anayestaafu Juni, 2016 na Bw. Renatus Molla
ambaye naye anastaafu Februari, 2016 ambao
ni wazaliwa wa kijiji hicho ambao watabaki hapo
shuleni kuwafundisha watoto.
Aliongeza kuwa, Serikali ya kijiji na wanakijiji
kwa ujumla watatafuta wenyewe walimu ili
waongeze nguvu shuleni hapo.
"Kwakuwa wanakijiji ndio waliosababisha hayo,
watafute wenyewe walimu wa kuwafundishia
watoto wao kama ni wanafunzi waliomaliza
kidato cha nne na cha sita wakubaliane,
mshahara wawalipe wao kwa sababu walimu
walioletwa na Serikali, hawahitajiki kijijini,"
alisema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walimu
wazawa kijijini hapo ambao inadaiwa ndio
watabaki kufundisha watoto, walisema hawako
tayari kurudi kufundisha shuleni hapo na kama
mwajiri alikuwa na mpango wa kuwafukuza kazi
afanye hivyo si kurudi Nambaza.
Bw. Mafuru alisema jana alifuatwa na watu
ambao walimtukana, kumtemea mate na
kutishia kumuua tukio ambalo ameliripoti polisi
sasa kwanini aendelee kukaa kijijini hapo.
"Mimi ni mzawa wa kijiji hiki lakini ni mtumishi
wa Serikali kama walivyo watumishi wengine,
utumishi wangu ndio umesababisha nitendwe
vibaya, nitishiwe kuuawa na kuonekana sifai na
adui miongoni mwa wanakijiji, natishiwa sasa
iweje niendelee kuwepo kijijini.
"Nambaza sitakiwi tena nitauawa, uhai wa
maisha yangu ni bora kuliko kazi, kama mwajiri
anataka kunifukuza kazi afanye hivyo lakini
siwezi kurudi Nambaza kufundisha," alisema.
Kwa upande wake, Molla alisema, hawezi kurudi
kufundisha Nambaza kwani amevumilia mengi
pamoja na kumpoteza mtoto wake katika
mazingira ya kishirikina lakini bado anatishiwa
kuuawa hivyo ni bora afukuzwe kazi akafanye
shughuli nyingine kama mwajiri anaona
kumbakiza kijijini hapo atakuwa amemtendea
haki kwa sheria za utumishi.
"Sitarudi Nambaza, nipo tayari kufukuzwa kazi,
mizigo na familia yangu nimeitoa Nambaza
baada ya kutendwa vibaya na wanakijiji,
nimetishiwa kifo na hao hao wanakijiji, kurudi
hapo ni kwenda kufa, siwezi kufuata kifo
ninachokiona hadi Mwenyezi Mungu
atakapoamua," alisema.
Aliongeza kuwa, mwaka 2014 mwanaye alikufa
katika mazingira ya kutatanisha kishirikina
kwani hakuugua bali alianguka njiani akitembea
na kufa papo hapo.
Mwalimu Munaku, ambaye tayari
amekwishajiondosha kijijini hapo akihofia
kuuawa kutokana na vitisho kutoka kwa
wanakijiji, hakuweza kupatikana ili kuzungumza
kama yuko tayari kuendelea kufundisha shuleni
hapo ama la.

posted from Bloggeroid

No comments