Header Ads

MBINU ZA KUWA NA UTAJIRI WAKUDUMU

BILA shaka ukiulizwa leo kama unataka kuwa
tajiri, jibu lako litakuwa ni NDIYO! Lakini je,
tunaelewa maana ya utajiri na namna ya
kuwa tajiri? Hili ni swali ambalo majibu yake
yanawasumbua wengi . Mada hii itakusaidia
kupata mwanga wa maana na namna ya
kuutafuta utajiri .
Wengi wanaamini kuwa ili mtu awe tajiri
lazima awe na bahati ya kipekee . Watu
wengi hudhani kuwa hawawezi kuwa matajiri
mpaka watumie mizizi ya Bagamoyo , Tanga
au Sumbawanga . Wengine huamini kwamba
ili uwe tajiri, ni lazima uoe au uolewe na
tajiri. Zipo imani nyingi juu ya utajiri, wengine
wanaamini lazima uwe na ‘ zali ’, ufanye
biashara ya magendo, ukwepe kodi , uibe,
utoe uhai wa mtu au utumie njia nyingine
haramu ndiyo uupate utajiri.
SIRI YA UTAJIRI HII HAPA
Siri kubwa ya mtu kuufikia utajiri wa kweli na
wa kudumu , ni kuanzisha biashara yenye
faida ambayo utakuwa na uwezo wa kuimiliki
na siyo biashara ikumiliki wewe . Ukifanikiwa
kuanzisha biashara yako , jambo la muhimu
kuliko yote ni kuhakikisha unaipangilia ili
iweze kujiendesha au kuendeshwa na watu
wengine bila wewe kuhusika nayo moja kwa
moja lakini kila kitu kiwe chini ya usimamizi
na udhibiti wako .
Ukiwa na biashara inayojiendesha yenyewe ,
utakuwa na uwezo wa kuanzisha biashara
nyingine zaidi , yaani ya pili . Hii ya pili ikifikia
uwezo wa kujiendesha kama ile ya awali ,
sasa utakuwa na uwezo wa kufungua
biashara ya tatu n . k .
Biashara ni kama mchezo fulani unaosisimua
na inatakiwa ufurahie mchezo huo . Hivyo
ndivyo wafanyavyo wajasiriamali wakubwa
duniani kama akina Salim Bhakhresa na
Reginald Mengi kwa hapa Tanzania , Aliko
Dangote wa Nigeria, Mukhesh Dhirubai
Ambani wa India , Carlos Slim wa Mexico au
Richard Brandson wa Uingereza mwenye
makampuni zaidi ya mia tatu .
Jambo la kutia moyo ni kwamba , unaweza
kujifunza kufanya hivyo . Kumbuka kuwa
hakuna aliyezaliwa anajua kufanya kitu
chochote hapa duniani zaidi ya kulia , mara
tu tulipozaliwa. Kila tunachokifanya ,
tumejifunza baada ya kuwa wenyeji hapa
duniani. Vivyo vivyo, kila kitu hapa duniani ,
ukiwa na nia ya kweli, unaweza kujifunza
mpaka ukafanikiwa na kuwa mtaalam .
Ni vizuri kufahamu pia kwamba, sio lazima
uwe na biashara nyingi ili uwe tajiri. Wapo
wajasiriamali wengi mabilionea ambao
wanafanya biashara moja tu ambayo utakuta
imepanuka na kuwa kubwa katika nchi
iliyomo au imefanikiwa kupata masoko
mpaka nchi za jirani au hata za mbali.
Lengo la makala haya si kukwambia uwe
kama Bill Gates au Warren Buffett ( matajiri
namna mbili na tatu duniani kwa sasa ) au
uwe na hela kuliko watu wote barani Afrika
au Tanzania , japo hayo yote yanawezekana .
Lengo ni kukufundisha namna ya kubuni ,
kuanzisha , kuendesha na kuipangilia biashara
yako mpaka ifike hatua ya kujiendesha
yenyewe .
Shauku yangu kama mwandishi wa
ujasiriamali ni kukusaidia wewe msomaji kwa
kukupa maarifa yatakayokufanya uanze
biashara hata bila fedha au kwa mtaji mdogo
ili hatimaye uwe na uhuru wa kifedha na
muda , uishi upendavyo na usiteseke uzeeni.
Nitakufundisha mbinu , mikakati na maarifa
ambayo yatakufanya uwe mmiliki hodari wa
biashara na mwekezaji mkubwa.
USIKUBALI MTU AKUCHAGULIE KESHO
YAKO
Wakati wa uhai wako , kipawa kikubwa kuliko
vyote ulivyonavyo ni kipawa cha kufanya
uchaguzi wa kufanya mambo mbalimbali
ikiwemo mtindo wa maisha unaotaka kuishi .
Baadhi ya mambo mazuri ambayo unaweza
kuyafanya unapokuwa na uhuru wa kifedha
na muda ni kama vile ;
• Kusafiri na kuishi kokote ulimwenguni
wakati wowote upendapo.
• Kujisomesha na kujilipia karo katika chuo
chochote popote ulimwenguni.
• Kutembelea maajabu mbalimbali
ulimwenguni.
• Kusoma vitabu vya riwaya , vya maendeleo
binafsi au vyovyote uvipendavyo kwa uhuru.
• Kutumia muda wako kwa ndugu au marafiki
wa muhimu zaidi .
• Kwenda kutazama mechi za kimataifa za
michezo mbalimbali popote pale ulimwenguni
na burudani zingine za aina mbalimbali .
• Kujifunza kuimba na kutoa CD yako kwa
kuwa una muda na kipato cha kufanya hivyo .
• Kuogelea au kujifunza kuogelea na
kufurahia uumbaji wa Mungu .
• Kuwatembelea wazazi wako mara kwa
mara kadiri upendavyo .
Haya na mengine mengi , huwezi kuyafanya
kama huna uwezo wa kifedha na muda hivyo
ni muhimu kila mmoja akajifunza namna ya
kutafuta fedha ili ayafurahie maisha.

No comments