IGP AIBIWA UPANGA WA DHAHABU
Jeshi la Polisi limeingia katika kashfa
nzito baada ya mkuu wake, Inspekta Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga
wa dhahabu ambao ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa
nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO).
Upanga huo wenye uzito wa takriban kilo
tatu na wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni
kielelezo kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.
hdg
Mwaka jana Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa
SARPCCO, ambapo upanga huo ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali
Magwashi Victoria 'Riah' Phiyega, ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi
wa Afrika Kusini aliyekuwa amemaliza muda wake kwa wakati huo.
Hilo ni tukio la pili la wizi la mali
zinazohusu ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana ndani ya ofisi hiyo kuliibwa
kompyuta ndogo (laptop), ikiwa na taarifa muhimu za kipolisi. Hadi sasa
hakuna taarifa za kupatikana kwa kompyuta hiyo.
IGP Mwema alikabidhiwa upanga huo
Septemba 5, 2012, katika mkutano saba wa SARPCCO uliofanyika Zanzibar na
kuhudhuriwa na wakuu wa majeshi ya Polisi kutoka nchi 13, pamoja na
mashirika ya kimataifa.
Upanga huo ambao unakwenda sambamba na
bendera ya SARPCCO, ni moja ya vielelezo vya nchi iliyochaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ambaye moja kwa moja anakuwa ni Mkuu wa
Jeshi la Polisi katika nchi husika.
Kwa mujibu wa taratibu za SARPCCO,
vielelezo hivyo hutakiwa kuwekwa ofisini kwa kiongozi husika, ikiwa ni
alama ya kila mgeni atakayeingia ofisini hapo kutambua uwepo wa wadhifa
huo wa kimataifa.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa
IGP aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki iliyopita, wakati akijiandaa
kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa SARPCCO, ambaye ni IGP wa
Namibia.
Taarifa za ndani ya jeshi hilo zilibaini
kuwa, IGP alilazimika kuondoka bila upanga huo alipokwenda Namibia wiki
iliyopita kuhudhuria mkutano wa nane wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili
iliyopita mjini Windhoek.
Kwa mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema
alikabidhi upanga unaofanana na huo ambao siyo wa dhahabu, alioazimwa
kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni
Jenerali Sebastian Ndeitunga, na kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa
uenyekiti wa SARPCCO kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Uchunguzi ulibaini kuwa IGP Mwema alitoa
ahadi ya kurejesha upanga halisi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, au
Serikali ya Tanzania italazimika kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa
kashfa hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa
pamoja na dereva wake, ikidaiwa kuwa upanga huo baada ya kupokewa na IGP
Mwema, Septemba mwaka jana uliwekwa kwenye gari la kamishna
huyo.Kamishna Mussa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya
Mkutano wa Saba, na pia ofisa mwenyeji kwa wajumbe wa mkutano huo
uliofanyika Zanzibar.
Hata hivyo, taarifa zingine zilidai kuwa
IGP Mwema naye analaumiwa kwa kutofuatilia kwa karibu zana za kazi,
kwani baada ya kuupokea alitakiwa kuhakikisha unakuwepo ofisini kwake
kama alama ya uenyekiti wake.
Gazeti hili lilipowasiliana kwa njia ya
simu na Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa kuhusu madai
hayo alisema, kitara (upanga) hicho ni kweli kimepotea, lakini yeye
hahusiki kwa kuwa kila kitu kina utaratibu wake.
"Ni kweli kitara kilikabidhiwa kwa afande
IGP na mimi nilishuhudia kikikabidhiwa, na ni kweli kitara hakijulikani
kiliko, lakini mimi sihusiki na kupotea kwake. Ni kweli mimi nilikuwa
ofisa mwenyeji wa mkutano huo, lakini siku hiyo zilitolewa zawadi
nyingi, watu walipewa mikoba, kwa hiyo mtu akipoteza mkoba wake niulizwe
mimi?" alihoji Kamishna Mussa.
Alisema kila kitu kina utaratibu wake na
kwamba taarifa kwamba yeye amehojiwa kutokana na upotevu wa kitara hicho
au kuna kamati imeundwa, hazina ukweli.
"Sijawahi kuona kamati hiyo. Kamati hiyo
kwanza imeundwa na nani na inatoka wapi? Hayo maneno yanatengenezwa na
watu wa nje," alisema Kamishna Mussa.
Alisema kinachofanyika hivi sasa ni kukitafuta ili kiweze kurejeshwa kunakohusika.
Taarifa zingine zilidai hata bendera ya
mezani ya mwenyekiti wa SARPCCO, aliyokabidhiwa sambamba na upanga huo
nayo kuna hatihati ilipotea.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema aulizwe kamishina wa polisi Zanzibar.
"Suala hilo muulize Kamishina wa Zanzibar ndiye anayejua," alisema Senso.
Uchunguzi unaonyesha kuwa maofisa katika
ofisi ya IGP na ile ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, wamehojiwa akiwamo
Kamishna Mussa, na kwamba upelelezi mkubwa umekuwa ukiendelea ndani ya
jeshi hilo.
Hata hivyo, juhudi za gazeti hili za
kutaka kufahamu uamuzi wa SARPCCO katika ofisi yake ya uratibu iliyopo
kwenye ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Polisi wa Kimataifa (INTERPOL),
Harare, Zimbabwe, hazikuzaa matunda baada ya baruapepe iliyotumwa kwa
ofisa mratibu wa SARPCCO ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Kanda ya
INTERPOL, C. Simfukwe kutopata majibu.SARPCCO ilianzishwa mwaka 1995,
Victoria Falls, Zimbabwe, lakini kisheria ilitambulika rasmi mwaka 2006
na lengo lake kuu ni kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka.
Uenyekiti wake ni mwaka mmoja, ambapo kwa
sasa mwenyekiti ni Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia Inspekta
Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, aliyepokea wadhifa huo
kutoka kwa IGP Mwema.
CHANZO MWANANCHI.
Post a Comment