Dr. Slaa Aanza Rasmi Kumpigia Kampeni Magufuli......Asema Lowassa Hafai Kuwa Rais
Siku chache baada ya chama cha ACT-Wazalendo kutoa tamko rasmi kuwa
hawataweza kumruhusu Dk. Wilbroad Slaa kupanda kwenye jukwaa lao kumnadi
mgombea urais wa chama hicho kwa sababu za kiusalama, jana mwanasiasa
huyo ameanza rasmi kumpigia kampeni mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk.
John Magufuli.
Akiongea jana kupitia Star TV , Dk. Slaa aliweka wazi mtazamo wake kuwa
Dk. Magufuli ndiye anayefaa kuwa rais wa Tanzania kwa kulinganisha wote
waliojitokeza kugombea nafasi hiyo.
Dk. Slaa alisema kuwa amengalia kigezo cha mtu anayeweza kupambana na
ufisadi na amempa Dk. Magufuli asilimia 90 katika kigezo hicho.
“Ninasema sitamung’unya maneno, mimi nafikiri, baada ya kusikiliza
mikutano michache ambayo nimeweza kusikiliza, na baada ya kuona clips
mbalimbali kwa sababu siku hizi unaweza kuishi kwenye mwezi lakini
ukapata taarifa ya kila mahali. Kwa hiyo mimi Napata taarifa kokote
nilipo.
“Kwa kutazama yote hayo, mimi ambaye nimeendesha mapambano ya ufisadi
ninatafuta rais ambaye atatuondoa kwenye ufisadi. Sasa aliyeniridhisha
kwenye mapambano hayo baada ya kuona vigezo ni Magufuli. Sina njia
nyingine ni lazima nichague mmoja. Na kumbuka tunapochagua rais
hatuchagui vyama.. na haina maana kwamba mimi ni CCM, sina chama,
“Na tunapokwenda kwenye chumba cha kura tukumbuke tunamchagua kiongozi
wa nchi, tusiangalie huyu ni wa chama gani. Je anatufaa au hatufai,
anatufaa kwa nini. Kwenye vigezo vya rushwa, Magufuli nampa asilimia
90.”
Kadhalika, Dk. Slaa alieleza kuwa amekuwa akisikiliza sera za wagombea
hao lakini anaona mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa anatoa hotuba
isiyozidi dakika 10 bila kufafanua zaidi hivyo anaona hafai kuwa rais.
Dk. Slaa alitangaza kustaafu siasa baada ya kujiuzulu nafasi ya Ukatibu
Mkuu wa Chadema na kuachana na chama hicho kwa kile alichokieleza kuwa
ni hakuridhishwa na uamuzi wa chama chake hicho cha zamani kumpokea
Edward Lowassa.
Hata hivyo, Dk. Slaa alikiri kuwa yeye ndiye aliyepeleka wazo la
kumkaribisha Lowassa kwenye chama hicho baada ya jina lake kukatwa na
CCM mjini Dodoma na kunyimwa nafasi ya kugombea urais.
Dk. Slaa alieleza kuwa wazo hilo alilitoa kwa Askofu Josephat Gwajima wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, ambaye alimtaja kama ‘mshenga’.
Juzi, akiwa katika jimbo la Karatu, Dk. Magufuli alimsifia Dk. Slaa na kumuita mtu safi na shujaa.
Post a Comment