Serikali yatangaza Operesheni Kamata Makahaba na wateja wao

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetangaza
kuiunga mkono Polisi nchini katika operesheni ya kukamata wateja wa
makahaba kuhakikisha biashara hiyo inakoma nchini.
Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu alisema takwimu zinaonesha wanawake
ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Ukimwi, ambapo kati ya Watanzania
10 wanaopimwa, sita ni wanawake na wanaume ni wanne pekee.Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Dar es Salaam
jana, Ummy alisema si haki kuwakamata wanawake wanaojiuza na kuwaacha
wateja wao ambao ni wanaume.
“Ninalipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo kwa sababu imeonesha
kutoegemea upande mmoja kwa kuwakamata wanawake makahaba. Wote
wanaojiuza na wanaonunua huduma hiyo ni wakosaji wanaostahili
kuchukuliwa hatua za kisheria.Tunaungana na Polisi kushiriki operesheni
hiyo,” alisema.
Alieleza kuwa, biashara ya ukahaba inayofanywa na wanawake isingekuwepo
endapo wateja wasingekuwepo, hivyo, wateja wanastahili kukamatwa pia kwa
sababu ndio wanaoichochea.
Ummy alisema familia nyingi zina misukosuko na wanawake wengi wamekuwa
wakiteseka na wengine kuambukizwa magonjwa na waume zao wanaoshiriki
biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, alisema sasa wanataka kuona idadi ya wanaume
wateja wa biashara hiyo inatajwa sambamba na ya wanawake wanaokamatwa
nao ili ndugu na wake zao wafahamu kuhusu tabia yao hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, alisema hatua ya
kukamata wateja na wauza miili imetokana na makubaliano yaliyofikiwa na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Dar es Salaam.
Post a Comment